Urusi
| |||||
Kaulimbiu ya taifa: none | |||||
Wimbo wa taifa: Hymn of the Russian Federation | |||||
Mji mkuu | Moscow | ||||
Mji mkubwa nchini | Moscow | ||||
Lugha rasmi | Kirusi | ||||
Serikali | Jamhuri, Shirikisho serikali ya kiraisi Dmitry Medvedev Vladimir Putin | ||||
Uhuru {{{established_events}}} |
{{{established_dates}}} | ||||
Eneo - Jumla - Maji (%) |
17,075,400 km² (ya 1) 13 | ||||
Idadi ya watu - 2014 kadirio - 2002 sensa - Msongamano wa watu |
143,800,000 (ya 9) 145,164,000 8.3/km² (ya 217) | ||||
Fedha | Rubl (RUB )
| ||||
Saa za eneo - Kiangazi (DST) |
(UTC+2 to +12) (UTC+3 to +13) | ||||
Intaneti TLD | .ru, (.su reserved) | ||||
Kodi ya simu | +7
- | ||||
1 Rank based on Aprili 2006 IMF data |
Urusi (Россия Rossiya) ni nchi ya Ulaya ya Mashariki na Asia. Mji mkuu ni Moscow. Ni nchi kubwa duniani kieneo, ikiwa na km² 17,075,400. Kuna wakazi 144,000,000.
Urusi imepakana na Norway, Ufini, Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Belarus, Ukraine, Georgia, Azerbaijan, Kazakhstan, China, Mongolia na Korea ya Kaskazini. Iko karibu vilevile na maeneo ya Marekani (jimbo la Alaska liko ng'ambo ya mlango wa Bering) na Japani (kisiwa cha Hokkaido kiko ng'ambo ya mlango wa La Pérouse.
Hadi 1991 Urusi ilikuwa sehemu ya Umoja wa Kisovyeti na kiini chake. Wakati ule iliitwa Shirikisho la Jamhuri ya Kisovyiet ya Kijamii ya Kirusi.
Urusi ilikuwa udikteta chini ya chama cha kikomunisti. Tangu 1990 imekuwa demokrasia.
Muundo wa utawala ni shirikisho la jamhuri chini ya rais mtendaji.
Jiografia
Eneo la Shirikisho la Kirusi linajumlisha sehemu kubwa ya kaskazini ya mabara ya Ulaya na Asia. Umbali kati ya upande wa magharibi na upande mashariki kabisa ni karibu kilomita 8,000.
Mkoa wa Kaliningrad haufuatani moja kwa moja na maeneo mengine ya Urusi: umetengwa nayo na nchi za Kibaltiki.
Mara nyingi Urusi hutazamiwa kama sehemu mbili: Urusi wa Ulaya hadi milima ya Ural na Siberia au Urusi wa Kiasia ambayo ni nchi pana kati ya Ural na Pasifiki.
Pwani ndefu ya kaskazini inatazama Bahari ya Aktiki.
Sehemu kubwa ya Urusi ni tambarare penye vilima vidogo tu. Milima mirefu inapatikana kusini na mashariki mwa Siberia.
Hali ya hewa
Sehemu kubwa za Urusi huwa na vipindi vya majira tofauti sana; joto kubwa inafuatana na baridi kali.
Kaskazini mwa Siberia kuna ardhi iliyoganda milele maana yake baridi imeingia katika ardhi kabisa. Wakati wa joto sentimita za juu zinapoa na mimea kama nyasi na maua inastawi lakini hakuna miti mikubwa kwa sababu nusu mita chini ya ardhi halijoto iko daima chini ya =C°.
Mito
Kati ya mito mikubwa kuna:
- Volga ambayo ni mto mrefu wa Ulaya ukiishia katika Bahari ya Kaspi
- Dnepr unaoishia katika Bahari Nyeusi; ni njia ya maji muhimu
- Oka
- Moskva
- Ob
- Irtysh
- Yenisei
- Lena
- Neva
- Don
- Amur
Miji mikubwa
Majiji mawili makuu ni Moscow na Sankt Peterburg.
Moscow ni mji mkuu wa kale uliyorudishiwa nafasi yake baada ya mapinduzi ya kikomunisti ya mwaka 1918.
Sankt Peterburg ilikuwa mji mkuu kuanzia mwaka 1703 hadi 1918 kama makao makuu ya tsar au kaisari wa Urusi. Miaka 1924-1989 ikaitwa Leningrad kwa heshima ya Lenin, kiongozi wa mapinduzi.
Miji mingine mikubwa ni pamoja na:
Historia
Historia ya Urusi kama nchi ya pekee ilianza polepole pale ambako makabila ya wasemaji wa Kislavoni cha Mashariki walipoanza kujenga maeneo yao kuanzia karne ya 8 BK.
Waskandinavia waliunda dola la kwanza katika eneo la Kiev, wakalitawala kama dola la Kislavoni. Wenyewe waliingia haraka katika lugha na utamaduni wa wenyeji, lakini waliacha jina lao kwa sababu "Rus" kiasili ilikuwa jina la Waskandinavia wale kutoka Uswidi ya leo.
Mwaka 988 Kiev ilipokea Ukristo wa Kiorthodoksi kutoka Bizanti. Tukio hilo liliathiri moja kwa moja utamaduni na historia yote iliyofuata.
Dola la Kiev liliporomoka kutokana na mashambulio ya Wamongolia baada ya Jingis Khan, na maeneo madogo zaidi yalijitokeza yaliyopaswa kukubali ubwana wa Wamongolia.
Upanuzi wa utemi wa Moscow
Kubwa kati ya maeneo yale madogo ulikuwa utemi wa Moscow. Watemi wa Moscow walichukua nafasi ya kwanza kuunganisha Waslavoni wa Mashariki dhidi ya Wamongolia na kupanua utawala wao.
Baada ya anguko la Konstantinopoli mwaka 1453 watawala wa Moscow walipokea cheo cha Kaisari wa Roma kilichoitwa "tsar" na kuwa cheo cha watawala wa Urusi hadi mwaka 1917.
Mpaka karne ya 18 eneo la Moscow lilikuwa tayari kubwa likabadilika kuwa Milki ya Kirusi iliyoendelea kupanuka katika Siberia na Asia ya Kati, ikawa kati ya milki kubwa kabisa za historia ikienea kutoka Poland upande wa magharibi hadi bahari ya Pasifiki upande wa mashariki.
Matengenezo ya kisiasa chini ya Petro I
Tsar Petro I (1689 - 1725) alitambua ya kwamba nchi yake ilikuwa nyuma upande wa teknolojia na elimu kulingana na mataifa ya Ulaya. Alianzisha mabadiliko mengi ya kuiga mfano wa Ulaya ya Magharibi akahamisha mji mkuu kutoka Moscow kwenda mji mpya aliounda sehemu ya magharibi ya milki yake akauita Sankt Peterburg.
Tangu wakati wa Petro I nchi ilishiriki katika siasa ya Ulaya pamoja na vita vingi vya huko.
Mwanzo wa karne ya 19 milki ikashambuliwa na Napoleon Bonaparte aliyeteka Moscow lakini Warusi walifaulu kuwafukuza maadui kwa msaada wa baridi iliyoua askari wengi wa Ufaransa.
Upanuzi katika Asia
Matsar wa Urusi waliendelea kutawala kwa kuwa na mamlaka zote bila kushirikisha wananchi jinsi ilivyokuwa kawaida katika sehemu nyingine za Ulaya. Miji iliona maendeleo ya viwanda na jamii ya kisasa, lakini sehemu kubwa ya wakulima waliendelea kukaa chini ya utawala wa makabaila.
Katika sehemu ya pili ya karne ya 19 Urusi ulipanua utawala wake juu ya maneo makubwa ya Asia ya Kati na milima Kaukasus ukashindana na Milki ya Osmani, Uajemi na athira ya Uingereza katika Asia.
Mapinduzi za 1905 na 1917
Mwanzoni mwa karne ya 20 Urusi ukaonekana tena kuwa nyuma ya nchi za magharibi na sababu kuu ilikuwa nafasi kubwa ya serikali iliyojitahidi kusimamia mabadiliko yote katika jamii na kuzuia mabadiliko yaliyoonekana magumu machoni pa Tsar, pa makabaila na pa maaskofu wa Kanisa la Kiorthodoksi.
Mwaka 1904 upanuzi wa Urusi katika Asia uligongana na upanuzi wa Japan. Katika vita dhidi ya Japani Urusi ulishindwa na tukio hili lilisababisha mapinduzi ya Urusi ya 1905. Tsar Nikolas alipaswa kukubali uchaguzi wa bunge la duma kwa mara ya kwanza. Hata hivyo haki za duma zilikuwa chache na mabadiliko yalitokea polepole mno.
Urusi ulijiunga mwaka 1914 na vita kuu ya kwanza ya dunia ukisimama upande wa Uingereza na Ufaransa dhidi ya Ujerumani na Austria-Hungaria. Vita havikuenda vizuri, wananchi wakaona njaa na mapinduzi ya Februari 1917 yakamfukuza Tsar aliyejiuzulu.
Vita vikaendelea na Wajerumani walizidi kusogea mbele. Serikali mpya ya bunge ikapinduliwa katika mwezi wa Oktoba 1917 na mapinduzi ya Bolsheviki chini ya kiongozi wao Vladimir Ilyich Lenin.
Utawala wa kikomunisti na Umoja wa Kisovyeti
Huo ulikuwa mwanzo wa vita ya wenyewe kwa wenyewe. Wakomunisti chini ya Lenin walishinda na kugeuza Urusi kuwa Umoja wa Kisoveti tangu mwaka 1922, wakitawala kwa mfumo wa kiimla wa chama chao. Ili kurahisisha utawala wao Wakomunisti waliamua kutawala Urusi wa awali kwa muundo wa shirikisho, wakaunda jamhuri mbalimbali kufuatana na mataifa ndani ya eneo hilo kubwa.
Urusi lilikuwa sasa jina la jamhuri kubwa katika umoja huu nao ukaitwa Shirikisho la Jamhuri ya Kisovyiet ya Kijamii ya Kirusi.
Kikatiba jamhuri hizo zote zilikuwa nchi huru lakini hali halisi zilitawaliwa zote kutoka makao makuu ya chama cha kikomunisti huko Moscow. Katiba hiyo ilipata umuhimu tangu 1989, wakati wa mwisho wa utawala wa Wakomunisti ambako jamhuri zote zilitafuta uhuru wao zikaachana na Umoja.
Mji mkuu Sant Peterburg ulibadilishwa jina kuwa Leningrad na baadaye makao makuu ya nchi yakahamishwa tena kwenda Moscow.
Kiongozi aliyemfuata Lenin mwaka 1924 alikuwa Josef Stalin aliyeweza kugeuza utawala wa chama kuwa utawala wake mwenyewe akiongoza kwa jina la Katibu Mkuu wa chama cha kikomunisti.
Mwaka 1939, mwanzoni mwa vita kuu ya pili ya dunia Stalin alipatana na Ujerumani wa Adolf Hitler kugawa maeneo ya Poland na nchi za Baltiki kati yao lakini mwaka 1941 Hitler alishambulia pia Umoja wa Kisovyeti.
Warusi walipoteza askari milioni kadhaa, lakini waliweza kuwazuia Wajerumani wasiteke Moscow na Leningrad. Kwa msaada wa Marekani Warusi waliweza kurudisha jeshi la Ujerumani na kusogea magharibi. Umoja wa Kisovyeti ukawa kati ya nchi washindi wa vita kuu ya pili ya dunia.
Mashindano ya vita baridi dhidi ya Marekani
Tangu mwaka 1945 jeshi la Urusi lilikaa katika nchi zote za Ulaya ya Mashariki hadi katikati ya Ulaya. Katika nchi hizo zote serikali za kikomunisti zilianzishwa na kusimamiwa na ofisi kuu ya chama cha kikomunisti huko Moscow.
Urusi ulikuwa kiongozi wa nchi za kijamaa, ukishindana katika vita baridi dhidi ya nchi za magharibi zilizoongozwa na Marekani. Athira ya Umoja wa Kisovyeti ilipanuka hadi Afrika, Asia na Amerika ya Kati ambako nchi mbalimbali zilianza kuiga mtindo wa kikomunisti.
Kusambaratika kwa Umoja kwa Kisovyeti
Utawala wa kikomunisti uliendelea hadi mwaka 1990. Mwishoni matatizo ya uchumi yalizidi kwa sababu mfumo wa uchumi ulioongozwa moja kwa moja na serikali kuu, pamoja na utaratibu wa kiimla uliozuia wananchi kupinga siasa ya viongozi na kuleta hoja tofauti, ulisababisha tena nchi kubaki nyuma.
Tangu mwaka 1990 jamhuri kadhaa za Umoja wa Kisovyeti ziliondoka katika umoja na kutangaza uhuru wao ilhali serikali ilishindwa nguvu ya kuwazuia. Mwaka 1991 jamhuri wanachama za mwisho Urusi, Belarus na Ukraine ziliamua kumaliza Umoja wa Kisovyeti.
Urusi mpya
Tangu mwaka 1991 Urusi ulipungukiwa na maeneo mengi yaliyotwaliwa katika karne ya 19 na ya 18, ukabaki peke yake ingawa bado ni dola kubwa kuliko yote duniani.
Marais wa Urusi baada ya 1991 walikuwa Boris Yeltsin na Vladimir Putin.
Dmitry Medvedev alichaguliwa kuwa rais wa Urusi mwaka 2008 na mtangulizi wake Vladimir Putin akawa waziri mkuu.
Siasa
Utawala
Kulingana na katiba ya nchi, Urusi ni shirikisho na jamhuri ambako rais ni mkuu wa nchi [1]na waziri mkuu ni kiongozi wa serikali.
Shirikisho la Urusi linafuata muundo wa demokrasia yenye mfumo wa vyama vingi. Kuna serikali ya kiraisi yenye mikono mitatu:
- Bunge: kuna sehemu mbili ambayo moja ni duma ya Urusi yenye wabunge 450 na Halmashauri ya Shirikisho la Urusi lenye wawakilishi 166 waliochaguliwa na bunge za Maeneo ya Shirkisho la Urusi.
- Serikali: rais ni Amiri Jeshi Mkuu, anaweza kutoa veto dhidi ya sheria zilizoamuliwa na bunge, na kuteua baraza la mawaziri pamoja na maafisa wengine muhimu.
- Mahakama: Kuna Mahakama ya kikatiba, Mahakama Mkuu na mahakama nyingine za ngazi za shirikisho na majaji wanachaguliwa na HAlmashauri ya Shirikisho kufuatana na mapendekezo ya rais.
Rais huchaguliwa kwa kura ya wananchi wote kwa kipindi cha miaka sita akiweza kurudishwa mara moja madarakani; anaweza kugombea tena baada ya kupumzika angalau kipindi kimoja. [2]
Baraza la mawaziri lina waziri mkuu na mawaziri wake wanaoteuliwa na rais kulingana na pendekezo ka waziri mkuu. Waziri mkuu anahitaji kukubaliwa na duma.
Vyama vya kisiasa muhimu ni Urusi wa Umoja, Chama cha Kikomunisti cha Urusi, Chama Huria cha Urusi na Urusi wa Haki.
Mfumo wa Shirikisho
Kuna Maeneo ya Shirikisho la Urusi 85.
Kulingana na katiba ya nchi kuna maeneo 85 yanayofanya shirikisho lake. [3] pamoja na eneo la Krim na mji wa Sevastopol.[4]
Maeneo ya shirikisho yanawakilishwa sawa katika bunge na kila moja inapewa wawakilishi wawili. [5] Lakini hali halisi yana viwango tofauti ya madaraka ya kujitawala katika siasa ya ndani.
- Jamhuri za shirikisho 22 ambazo kwa jina zinajitawala, zina katiba zao zikiwa na gavana na bunge zinazochaguliwa moja kwa moja na wakazi wake. Sheria ya Urusi inaamuru uchaguzi wa moja kwa moja wa wakuu wa jamhuri lakini hwaruhusiwi tena kutumia cheo cha "raisi".[6] Jamhuri ina haki ya kujiamulia kuhusu lugha rasmi. HAdhi ya jamhuri ilianzishwa kutokana na kuwepo kwa kabila kubwa au taifa lenye utamaduni usio wa Kirusi. Hali halisi jamhuri nyingi zina wakazi wengi Warusi kutokana na historia ya uhamiaji katika zamani za Umoja wa Kisovyeti.
- Mikoa ya Urusi ni 55 na kuna majina mawili kwa mikoa hii. Mingi inaitwa oblast ambayo ni hali ya kawaida na 9 inaitwa krai ka sababu za kihistoria; zote zina gavana na wabunge wanaochaguliwa na wakazi moja kwa moja.
- Majiji ya Shirikisho 3 ambayo ni majiji yaliyopewa hadhi ya pekee kutokana na umuhimu wao wa kitaifa (Moscow, Sankt Petersburg na Sevastopol)
- Maeneo huru 5 ambayo ni maeneo makubwa penye watu wachache yaliyopewa hadhi ya pekee kwa sababu ni maeneo ya kidesturi ya wenyeji asilia wasio Warusi; sku hizi kote Warusi wamekuwa wengi lakini hadhi ya eneo huru ni jaribio la kuonyehsa heshima kwa utamaduni wa pekee wa wenyeji asilia. "Uhuru" katika mengi ni kwa jina tu, mengi hutawaliwa kiutawala na mkoa wa jirani na uhuru unahusu zaidi utamaduni na kutunza lugha a wenyeji asilia. MAeneo manne huitwa "okrug" huru na moja "oblast huru" ambayo ni Oblast huru ya Kiyahudi)
Maeneo yote ya Shirikisho yamepangwa katika kanda 9. Kila moja huwa na Mkuu wa Kanda anayeteuliwa na raisi na kazi yake ni kusimamia na kuangalia kazi ya serikali za maeneo.
Watu
Warusi asilia ni 81%, lakini kuna makabila mengine 160 katika shirikisho, ambayo yanatumia lugha 100 hivi. Kubwa zaidi ni la Watatari (3.7%) wanaoongea Kitatari.
Lugha rasmi na ya kawaida ni Kirusi.
Baada ya ukomunisti kuanguka, dini ulizozipiga vita kwa njia zote kwa miaka mingi zimepata uhai mpya. Siku hizi 3/4 za wakazi ni Wakristo, hasa Waorthodoksi, na 6.5% ni Waislamu.
Tanbihi
- ↑ "The Constitution of the Russian Federation". (Article 80, §1). Iliwekwa mnamo 27 Desemba 2007.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "The Constitution of the Russian Federation". (Article 81, §3). Iliwekwa mnamo 27 Desemba 2007.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "The Constitution of the Russian Federation". pravo.gov.ru (kwa Russian). 11 Aprili 2014. ku. 19, 21.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) CS1 maint: unrecognized language (link) - ↑ "Treaty Between the Russian Federation and the Republic of Crimea on Ascension to the Russian Federation of the Republic of Crimea and on Establishment of New Subjects Within the Russian Federation" (kwa Kirusi). Kremlin.ru. 18 Machi 2014. Iliwekwa mnamo 10 Aprili 2014.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "The Constitution of the Russian Federation". (Article 95, §2). Iliwekwa mnamo 27 Desemba 2007.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Federal Law of 28.12.2010 No. 406-FZ
Viungo vya nje
- Urusi katika Open Directory Project
- Wikimedia Atlas of Russia
- Russia entry at The World Factbook
- Russia at UCB Libraries GovPubs
- Russia from the BBC News
- Russia at Encyclopædia Britannica
- Serikali
- Official Russian governmental portal
- Chief of State and Cabinet Members
- Russian News Agency "Ria Novosti"
- Vingine
- Uchumi wa Russia
- Post-Soviet Problems from the Dean Peter Krogh Foreign Affairs Digital Archives
- Russia Beyond the Headlines International news project about Russia
- Way to Russia. An Introduction to Russia and Russian People
- Russia cities and regions guide
- Official Russia Travel Guide
- Russian Consulate
- Russia Beyond the Headlines International news project about Russia
- Moscow Russia Insider's Guide Moscow and Russia through Muscovite's eyes.