[go: up one dir, main page]
More Web Proxy on the site http://driver.im/Nenda kwa yaliyomo

Uhuru wa taaluma

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Uhuru wa taalumu humaanisha haki mbalimbali za binadamu pamoja na wajibu wa pekee vinavyostahili kupatikana kwa shughuli na maisha ya vyuo vikuu pamoja na mafundisho na uchunguzi wa sayansi kwa jumla.

Maana ya uhuru wa taaluma

[hariri | hariri chanzo]

Uhuru wa taaluma humaanisha hasa:

  • Uhuru wa uchunguzi: mtaalamu awe huru kuchunguza yale anayoyaona mwenyewe ni muhimu, kuchagua mbinu wa kuendesha uchunguzi wake, kufikia hitimisho anayoona sawa kutokana na uchunguzi wake na kulitangaza kwa njia anayochagua mwenyewe. Mipaka ya uhuru huu inaweza kuwepo kutokana na sheria za nchi kwa mfano hakuna uhuru wa kutesa watu kwa lengo la kufikia elimu mpya kuhusu tiba au biolojia.
  • Uhuru wa kufundisha: walimu na maprofesa wa Chuo kikuu wachague wenyewe ni habari na mawazo gani yanayolingana na fani yao watakayotumia katika mafundisho na masomo. Wawe huru kutangaza hitimisho na maoni yao yanayohusu fani bila kujali kama zinakubaliwa na jamii, siasa, serikali au dini.
  • Uhuru wa kujifunza: wanafunzi wa chuo kikuu wanastahili kushiriki katika uhuru wa taaluma kwa kuwa na kiwango cha uhuru kuhusu fani au mada za kozi wanatakazochagua na mitihani watakayofanya. Uhuru huu una mipaka yake kutokana na utaratibu wa masomo, hasa katika ngazi ya kwanza, lakini unatakiwa kupanuka kwenye ngazi za juu kama MA au udokta.

Sababu za uhuru wa taaluma

[hariri | hariri chanzo]

Kutambua dunia na hali halisi hutegemea na kupatikana kwa mifumo, mbinu na mawazo mengi iwezekanavyo kwa wachunguzi wengi bila mipaka.

Katika historia ya sayansi imeonekana ya kwamba miiko ya kijamii, ya kiutamaduni, ya kisiasa au ya kidini ni vikwazo kwa maendeleo ya sayansi na kwa kazi ya kuboresha elimu kwa jumla. Kwa hiyo jamii zilizokubali uhuru wa taaluma ziliendelea vizuri kuliko jamii zilizojaribu kupiga marufuku maswali, mafundisho au mbinu za uchunguzi fulani.

Mfano wa Lysenko

[hariri | hariri chanzo]

Kwa mfano katika mfumo wa ukomunisti serikali ya Umoja wa Kisovyeti (Urusi hadi 1990) ilijaribu kutawala kazi ya vyuo. Tokeo mojawapo lilikuwa mnamo miaka ya 1930 chini ya udikteta wa Stalin ya kuwa profesa mmoja wa biolojia, kwa jina Trofim Lysenko, aliyepinga mafundisho ya Mageuko ya spishi ya Darwin akidai nadharia yake ililingana na mafundisho ya chama cha kikomunisti. Wataalamu wengi wa Kirusi waliofundisha kinyume walifukuzwa kazi au hata kufungwa jela na matumizi ya nadharia yake yalisababisha uharibifu wa mavuno na hata kipindi cha njaa. Ukandamizaji wa majadiliano ya kitaalamu ulikuwa hasara kwa Urusi na pia China ya kikomunisti ambako nadharia ya Lysenko ilipokelewa.

Hali ya kisheria

[hariri | hariri chanzo]

Uhuru wa taaluma si sehemu ya sheria ya kimataifa. Kuna mapendekezo tu ya UNESCO ya mwaka 1997 yanayokazia haki ya walimu kwenye ngazi ya vyuo vikuu kuwa na uhuru wa taaluma ("academic freedom").[1].

Kuna nchi mbalimbali zilizoeleza uhuru wa taaluma katika katiba za nchi au sheria kuhusu vyuo vikuu. Mifano:

Nchi zinazokazia uhuru wa kitaaluma zinaachia vyuo pia mamlaka ya kujitawala katika shughuli za kutumia bajeti yake, kuteua maprofesa na kuamua juu ya silabasi za fani mbalimbali.

Hata hivyo nchi nyingi zinatunza haki ya serikali kuingilia kati kazi ya vyuo vikuu na kutumia taratibu mbalimbali za kuamulia kuhusu mafundisho mbalimbali, pia kuachisha kazi walimu kwa sababu za kisiasa.

Kanisa Katoliki liliweka utaratibu kwa vyuo vikuu vya kikatoliki katika tangazo "Sapientia Christiana" ("Hekima ya Kikristo") [2] linalokazia uhuru wa mafundisho na uchunguzi "wa kweli katika mipaka ya Neno la Mungu jinsi linavyofundishwa na Ualimu wa kanisa".

  1. Unesco: Recommendation concerning the Status of Higher-Education Teaching Personnel
  2. Sapientia Christiana