[go: up one dir, main page]
More Web Proxy on the site http://driver.im/Nenda kwa yaliyomo

Kaizari

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mfalme mkuu)
Julius Caesar alikuwa asili ya cheo cha Kaizari.
Kaizari Augusto wa Dola la Roma.
Mtawala wa Ufaransa Napoleon Bonaparte aliyejiwekea taji la Kaizari 1804.
Kaizari Bokassa mwaka 1977.

Kaizari ni cheo cha mfalme mkuu. Neno la Kiswahili limetokana na lugha ya Kijerumani "Kaiser", lakini asili yake ni Kilatini "Caesar".

Asili ya Kiroma

[hariri | hariri chanzo]

Asili ya cheo ni Julius Caesar aliyekuwa kiongozi wa Dola la Roma hadi kuuawa kwake na wapinzani mwaka 44 KK.

Watawala waliomfuata walianza kutumia jina la Caesar kwa heshima yake hadi jina likawa cheo.

Cheo cha Kaizari kiliendelea kutumika katika eneo la Dola la Roma ya Mashariki (Bizanti) hadi mwaka 1453.

Katika Ulaya yenyewe mfalme wa Wafaranki Karolo Mkuu alipokea cheo cha "Caesar" au Kaizari. Baadaye wafalme Wajerumani waliomfuata Karolo Mkuu katika sehemu ya mashariki ya ufalme wake waliendelea kutumia cheo hiki cha Caesar au Kaizari.

Neno la Kaizari liliingia katika lugha ya Kiswahili wakati wa ukoloni wa Kijerumani huko Tanzania, kwa kuwa Austria na Ujerumani zilitawaliwa hadi mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia 1918 na wafalme wenye cheo cha "Kaizari".

Vilevile mfalme wa Urusi alikuwa na cheo kilekile kilichoitwa "Tsar" kwa Kirusi, ilhali neno hili limeundwa pia kutoka "Caesar".

Lugha za Kiingereza na Kifaransa zilitumia cheo tofauti cha macaesar wa Kiroma, ndicho "Imperator" (= mwenye amri, mwenye mamlaka, jemadari) kilichokuwa "Emperor" kwa Kiingereza au "Empereur" kwa Kifaransa.

Nje ya Ulaya

[hariri | hariri chanzo]

Kaizari ni cheo cha mfalme aliye juu ya wafalme wengine. Kutokana na uzoefu huu hata Shah wa Uajemi, Tenno wa Japani, Huangdi wa China na Negus Negesti wa Ethiopia hutajwa kwa cheo cha "Kaizari".

Malkia Viktoria wa Uingereza alitumia cheo cha Kaizari ("empress") kama mtawala wa Uhindi tangu mwaka 1877.

Wakati wa ukoloni mtawala mkuu wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani alikuwa Kaizari Wilhelm II wa Ujerumani; kwenye sarafu ya rupia alionyeshwa pamoja cheo kwa lugha ya Kilatini "imperator".

Rais Jean-Bedel Bokassa alijitangaza kuwa Kaizari ("empereur") wa Afrika ya Kati mwaka 1977 akiiga mfano wa Napoleon Bonaparte aliyejiwekea taji la Kaizari ya Ufaransa mwaka 1804. Bokassa alipinduliwa mwaka 1979 na nchi kuwa jamhuri tena.