[go: up one dir, main page]
More Web Proxy on the site http://driver.im/Nenda kwa yaliyomo

Jaramogi Oginga Odinga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Oginga Odinga kwenye kitabu cha tawasifu yake.

Jaramogi Ajuma Oginga Odinga (1911 hivi – 20 Januari 1994) alikuwa mwalimu, mfanyabiashara, mwanasiasa na kiongozi wa Waluo nchini Kenya. Alikuwa makamu wa rais wa kwanza wa Kenya.

Maisha ya awali

[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa Bondo katika jimbo la Nyanza katika familia ya Kiluo. Baada ya kukamilisha elimu ya sekondari kwenye shule ya Alliance High School akaendelea kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere kule Uganda akawa mwalimu tangu mwaka 1939, baadaye pia mwalimu mkuu.

Odinga alijitahidi kujenga umoja kati ya Waluo wa Kenya pia huko Uganda na Tanzania. Akaheshimiwa na kuitwa "Ker" au kiongozi wa kiroho. Wakati ule alipewa jina la "Jaramogi" au "mwana wa Ramogi" aliyekuwa Ker katika karne ya 16 akikumbukwa sana kati ya Waluo.

Mwanasiasa

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1947 akaanzisha kampuni yake ya Luo Thrift and Trading Corporation. Mwaka uleule akaingia katika siasa akaitwa kuwa mjumbe wa baraza la ushauri wa koloni. Akajiunga na chama cha Kenya African Union.

Wakati wa vita ya Maumau Waingereza wakamkamata kiongozi Jomo Kenyatta, na Odinga alibaki kama mtetezi wa harakati ya kupigania uhuru.

Mnamo mwaka wa 1960 alikuwa kati ya waanzilishi wa chama cha KANU akampendekeza Kenyatta kuwa kiongozi wa chama. Kwa wakati huo Jaramogi alionekana mtu mwenye maono ya kuendesha nchi ya Kenya, lakini hakuwa na dhamira mbaya, alitaka Wakenya wawe na uongozi mwema usio na dhuluma yoyote.

Makamu wa Rais

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya uhuru Odinga alikuwa waziri wa mambo ya ndani, na tangu 1964 makamu wa rais Kenyatta.

Katika mawazo yake alionyesha mwelekeo upande wa ujamaa akaanza kupinga siasa ya viongozi wengine wa KANU walioelekea ubepari. Oginga alikuwa na moyo mkarimu na alitaka matakwa ya Wakenya yawe mstari wa mbele. Lakini sivyo KANU na Kenyatta walivyotaka, mchango wake wakati huo ulikuwa ni kutaka Wakenya waishi pasi na dhuluma yoyote. Hivi basi Kiongozi huyo shupavu alianza kutofautiana naye Kenyatta.

Upinzani

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1966 mkutano wa KANU ukafuta nafasi ya makamu wa mwenyekiti wa chama aliyoshika. Mnamo Aprili 1966 Odinga akajiuzulu katika serikali akaanzisha chama chake cha Kenya People's Union (KPU). Chama kipya kikateswa na serikali. Mwaka 1969 kulitokea ugomvi huko Kisumu wakati wa ziara ya rais Kenyatta, na Odinga alikamatwa na kutupwa jela kwa miezi 15.

Katika miaka ya 1970 Odinga alibaki upande wa upinzani. Baada ya kifo cha Kenyatta, rais mpya Daniel arap Moi alijaribu kumrudisha Odinga katika KANU na kumpa cheo kama mwenyekiti wa bodi ya kilimo. Lakini Odinga alipopinga siasa ya serikali uhusiano ulizorota. Odinga alijaribu kuunda chama kipya na wakati ule Kenya ikatangazwa kuwa nchi ya chama kimoja tu.

Mageuzi tangu 1990

[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa kuporomoka kwa utawala wa chama kimoja mnamo 1990/1991 Odinga alianzisha chama kipya cha NDP akatupwa tena jela na kuunda chama cha FORD kilichounganisha wapinzani wengi wa Moi.

FORD iliposambaratika mwaka 1992 Odinga akawa kiongozi wa kitengo kimoja akafikia nafasi ya nne katika uchaguzi wa rais wa 1992. Mafarakano yale ya upinzani yalimwezesha rais Moi kurudi kwa asilimia 35 za kura tu. Lakini kuundwa kwa FORD kulikuwa mwanzo wa mabadiliko yaliyosababisha mageuzi ya kisiasa kutokea katika uchaguzi wa mwaka 2002.

Odinga hakuona mafanikio hayo akaaga dunia katika Januari 1994.

Wana wawili wa mzee Odinga wamejihusisha na siasa pia, ni Raila Odinga na Oburu Odinga.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]


Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Jaramogi Oginga Odinga kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.