[go: up one dir, main page]
More Web Proxy on the site http://driver.im/Nenda kwa yaliyomo

Ukraini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ukraine)
Україна
Ukrayina

Ukraini
Bendera ya Ukraini Nembo ya Ukraini
Bendera Nembo
Kaulimbiu ya taifa: Slava Ukraini!
Wimbo wa taifa: Ще не вмерла України
Shche ne vmerla Ukrajiny
"Fahari ya Ukraini haijafifia"
Lokeshen ya Ukraini
Mji mkuu Kiev (Kyiv)
50°27′ N 30°30′ E
Mji mkubwa nchini Kiev
Lugha rasmi Kiukraini
Serikali Demokrasia
Volodymyr Zelensky
Denys Shmyhal
Uhuru
ilitangazwa
Kura ya maoni ya wananchi
ilikubaliwa
24 Agosti 1991
1 Desemba 1991
25 Desemba 1991
Eneo
 - Jumla
 - Maji (%)
 
603,700 km² (ya 44)
7%
Idadi ya watu
 - 2014 kadirio
 - 2001 sensa
 - Msongamano wa watu
 
44,291,413 (ya 32)
48,457,102
73.8/km² (ya 115)
Fedha Hryvnia ya Ukraine (UAH)
Saa za eneo
 - Kiangazi (DST)
EET (UTC+2)
EEST (UTC+3)
Intaneti TLD .ua
Kodi ya simu +380

-


Ramani ya Ukraini leo.

Ukraini (kwa Kiukraini: Україна, Ukrayina) ni nchi ya Ulaya ya Mashariki. Imepakana na Urusi, Belarusi, Polandi, Slovakia, Hungaria, Romania na Moldova.

Kuna pwani ya Bahari Nyeusi na ghuba ya Azov.

Mji mkuu ni Kiev (Kyiv).

Historia

Historia ya kale

Dola la Kiev, chanzo cha Urusi.

Vyanzo vya Ukraini ni pamoja na vile vya Urusi wakati ambako [[|kabila|makabila]] ya wasemaji wa Kislavoni cha Mashariki walikoanza kujenga maeneo yao kuanzia karne ya 8 BK.

Waviking kutoka Skandinavia waliunda miji ya biashara na dola la kwanza katika eneo la Kiev. Wenyewe waliingia haraka katika lugha na utamaduni wa Waslavoni wenyeji, lakini waliacha jina lao "Rus" ambalo kiasili lilikuwa jina la Waskandinavia wale kutoka Uswidi ya leo.

Mwaka 988 mtawala wa Kiev alipokea Ukristo wa Kiorthodoksi kutoka Bizanti. Aliagiza wananchi wabatizwe pamoja naye ambayo inakumbukwa kama "Ubatizo wa Urusi". Tukio hilo liliathiri moja kwa moja utamaduni na historia yote iliyofuata.

Dola la Kiev liliporomoka kutokana na mashambulio ya Wamongolia baada ya Jingis Khan waliovamia na kuchoma Kiev mnamo mwaka 1240. Milki iligawiwa na temi ndogo zilijitokeza zalizopaswa kukubali ubwana wa Wamongolia.

Baina ya Polandi, Lituanya na Utemi wa Moscow

Katika karne ya 14 sehemu kubwa ya maeneo ya Milki ya Kiev ya awali ilifikishwa chini ya utawala wa Polandi na Lituanya. Tawi moja la familia ya watawala wa Kiev lilidhibiti Moscow katika mashariki-kaskazini. Hapa viongozi wake walifaulu kuimarisha utawala na kupanusha eneo lake. Hata askiofu mkuu wa Kiev aliyepaswa kuondoka baada ya kuchomwa wa mji wake hatimaye alihamia Moscow. Hivyo watawala wa utemi wa Moscow walijitazama kama wafuasi halali wa Dola la Kiev wakaendelea kutumia jina "Rus" lililoendelea kuwa chumbukizo la jina Urusi. Hatimaye watemi wa Moscow walifaulu kushinda pia Wamongolia na kupata uhuru.

Maeneo makubwa ya Ukraini ya leo yalikuwa chini ya utawala wa Lituanya na Polandi na baadaye ya Ufalme wa Maungano ya Polandi-Lituanya. Mwaka 1696 watawala wa Polandi walishawishi sehemu ya maaskofu Waorthodoksi kukubali maungano na kanisa katoliki na hii ilikuwa chanzo cha kutokea kwa Kanisa Katoliki la Kigiriki la Ukraini.

Sehemu ya Ukraini upande wa mashariki wa mto Dnestr ilitawaliwa na Moscow.

Katika karne ya 18 Polandi iligawanywa kati ya majirani yake. Ugawaji huo uliongeza sehemu za Ukraini zilizofika chini ya utawala wa Urusi. Ila sehemu ya kusini-magharibi ilikuwa sehemu ya milki ya Austria. Katika maeneo chini ya Urusi Wakatoliki walipaswa kurudi katika Kanisa la Kiorthodoksi. Lakini katika maeneo yaliyochukuliwa na Austria tangu mwaka 1772, serikali iliwapa Wakatoliki Waukraini haki sawa na Kanisa la Kilatini; liliweza kuunda seminari na vyuo; taasisi hizo zikawa chimbuko la kukua kwa lugha ya Kiukraini na utaifa wa Kiukraini.

Karne ya 20

Miaka 1918 - 1921 baada ya mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na ya kuporomoka kwa Milki ya Urusi nchi ilikuwa na kipindi kifupi cha uhuru na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Baada ya ushindi wa wakomunisti, nchi iliungwa katika Umoja wa Kisovyeti kama kuwa Jamhuri ya Kisovyeti ya Kijamii ya Kiukraini kati ya 1922 - 1991 .

Baada ya mwaka 1927 Wakomunisti chini ya Stalin waliamua kufuta mali binafsi ya ardhi wakalazimisha wakulima wote kulima kw muundo wa ujamaa. Sisa hii ilisababisha njaa mbaya sana katika Ukraini kwenye miaka 1930-1932 ambamo Waukraini milioni 4 hivi walikufa njaa.

Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwenye Umoja wa Kisovyeti ilipiganiwa sana katika Jamhuri ya Kisovyeti ya Ukraini. Wajerumani waliua raia wa Kiyahudi milioni na nusu, kwa jumla walikufa Waukraini milioni 5-6 wakati wa vita.

Uhuru tangu 1991

Wakati wa kuporomoka wa ukomunisti Umoja wa Kisovyeti ilifutwa, hivyo Ukraini ilipata uhuru wake. Ndani ya nchi na siasa yake yalitokea mawazo tofauti kuhusu mwelekeo; walioshindana walikuwa hasa wale waliotaka kuelekea uanachama na Umoja wa Ulaya na wengine waliotafuta ushirikiano wa karibu zaidi na Urusi.

Mwaka 1991 Urusi na Ukraini ziliutia sahihi mkataba wa urafiki walipoahidiana kuheshimiana kama majirani wema.

Kwa msingi huo, mwaka 1994 Ukraini ilikabidhi Urusi silaha za nyuklia iliyowahi kurithi kutoka jeshi la Kisovyeti na kwenye Mkataba wa Budapest Urusi, Marekani na Uingereza ziliahidi kulinda Ukraini katika mipaka yake dhidi ya mashambulizi yoyote[1].

Hata hivyo, baada ya mwaka 2000 majadiliano ndani ya Ukraini kuhusu kujiunga na umoja wa NATO ilianza kuleta ugumu katika uhusiano na Urusi.

Mwaka 2013 yalitokea maandamano na mapigano kwa sababu rais Viktor Yanukovich aliamua ghafla kukataa mapatano ya kujiunga na Umoja wa Ulaya yaliyokwisha kukubaliwa tayari. Waandamanaji kwa mamia waliuawa na polisi na hatimaye rais alikimbilia Urusi. Hapo bunge liliamua kumwondoa madarakani na kuwa na uchaguzi mpya wa rais.

Katika hali hiyo Urusi ilivamia Krim kwa njia ya kuficha. Wanajeshi wasio na sare walitokea kwenye miji ya Krim wakivamia majengo ya serikali pamoja na bunge la kieneo[2]. Idadi isiyojulikana ya wabunge la jimbo la Krim waliamua tarehe 5 Februari kuondoa serikali ya jimbo wakaitisha kura za wananchi. Tarehe 11 Februari walitangaza uhuru wa Krim, na kura ya wananchi ya tarehe iliyoendeshwa na mamlaka mpya ilitangaza kuwa na kura nyingi za kujiunga na Urusi. Ombi hilo lilikubaliwa na Urusi.

Mnamo Aprili 2014 waandamanaji walivamia majengo ya serikali huko Donetsk wakidai pia kura kuhusu kujitenga na Ukraini. Baada ya kuondolewa na polisi, waandamanaji wenye silaha walitangaza maeneo ya Donetsk na Luhansk kuwa "jamhuri za kujitegemea". Serikali ya Ukraini iliongeza polisi na pia jeshi. Mapigano yalianza ambako jeshi la Urusi lilisaidia waasi, kwanza kwa siri na baadaye waziwazi. Mapigano hayo yalikuwa mwanzo wa Vita ya Donbas iliyoendelea hadi mwaka 2022.

Mwaka 2022 rais wa Urusi alitangaza kwamba yeye haoni Ukraini kama nchi halisi akaamuru jeshi lake kuvamia Ukraini tarehe 24 Februari.

Wakazi

Sensa ya mwaka 2001 ilionyesha ya kwamba 77.8% za wakazi hujiita "Waukraini". Waliojiita Warusi walikuwa 17.3%. Vikundi vingi vingine kama Wabelarusi, Wamoldova, Watartari, Wabulgaria, Wapolandi, Wayahudi na wengine walikuwa kila kimoja chini ya 1%.

Lugha

Kwa muda mrefu Ukraini ilitawaliwa na Urusi na Kirusi kilikuwa lugha ya utawala hali halisi. Hivyo wengi wamezoea Kirusi, hata kati ya Waukraini asilia; hivyo Kiukraini kilikuwa lugha mama ya 67.5%, Kirusi ya 29.6%.

Tangu uhuru serikali imeendesha sera ya kujenga lugha ya taifa, pamoja na kujali lugha nyingine 18 za kieneo.

Hivyo lugha rasmi ni Kiukraini (українська мова "ukrajin's'ka mova"), mojawapo kati ya lugha za Kislavoni, karibu sana na Kirusi, lakini angalau nusu ya wakazi hutumia pia Kirusi.

Dini

Baada ya ukomunisti kupiga vita dini kwa njia zote na kwa miaka mingi, siku hizi wakazi wengi wamerudia dini zao.

Walionayo ni hasa Wakristo (81.9%), wakiwemo wale wa Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi (23%), lakini Waorthodoksi wengine wamejitenga na kuanzisha Kanisa la Kiorthodoksi la Ukraini (40.8%).

Pia kuwa waamini wengiwengi wa Kanisa Katoliki (10.2%), hasa wa Kanisa Katoliki la Kigiriki la Ukraini (9.4%) linalofuata mapokeo ya Kigiriki kama Waorthodoksi, lakini pia wa Kanisa la Kilatini (0.8%).

Waprotestanti ni 2.2% na Waislamu 1.1%.

Pamoja na hayo, idadi ya wakazi inazidi kupungua haraka (-12.8% kati ya 1993 na 2014).

Tazama pia

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Ukraini kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. https://treaties.un.org/doc/Publication/UNTS/Volume%203007/Part/volume-3007-I-52241.pdf Memorandum on security assurances in connection with Ukraine’s accession to the Treaty on the Non-Proliferation of Nuclear Weapons, Tovuti ya treaties.un.org, iliangaliwa Machi 2022
  2. Gunmen Seize Government Buildings in Crimea, gazeti la New York Times ya 27 Februari 2014